Mahakama ya Los Angeles imeendelea kusikiliza ushahidi dhidi ya mwimbaji D4vd, anayefahamika kwa jina halisi David Anthony Burke, anayekabiliwa na mashtaka ya kumuua na kisha kuukatakata mwili wa Celeste Rivas Hernandez, aliyekuwa na umri wa miaka 14. Katika kikao cha mahakama kilichofanyika Julai 24, waendesha mashtaka waliwasilisha ujumbe wa simu unaodaiwa kuonyesha mazungumzo kati ya wawili hao kuhusu ujauzito na utoaji mimba wakati Celeste alipokuwa na umri wa miaka 13. Kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa na mpelelezi wa Idara ya Polisi ya Los Angeles (LAPD), Corey Farell, wawili hao walibadilishana ujumbe kadhaa uliogusia masuala ya uzazi wa mpango, kidonge cha dharura (Plan B), utoaji mimba na kuvunjika kwa uhusiano wao.
Waendesha mashtaka pia walidai kuwa zaidi ya picha 40 za unyanyasaji wa kingono dhidi ya mtoto zilipatikana kwenye simu ya Burke, pamoja na picha nyingine zinazodaiwa kuwaonyesha wawili hao katika matukio ya kingono. Kutokana na ushahidi huo, mama wa marehemu, Mercedes Martinez, alionekana kushindwa kuhimili hali hiyo na akaondoka nje ya ukumbi wa mahakama. Upande wa mashtaka unadai kuwa Burke alianza kuwasiliana na Celeste mwaka 2022 akiwa na umri wa miaka 11, huku uhusiano wa kingono ukidaiwa kuanza mwaka 2023 alipokuwa na miaka 13, wakati Burke akiwa na miaka 18.
Inadaiwa kuwa Aprili 23, 2025, Burke alimuua Celeste kufuatia ugomvi uliotokana na mahusiano yake na wanawake wengine, siku chache kabla ya kuachia albamu yake ya kwanza. Mahakama pia ilielezwa kuwa mwezi mmoja kabla ya kifo chake, Celeste alimwandikia Burke akitaka uhusiano wao ubaki wa mtandaoni pekee, akisema alihisi maisha yao yalikuwa yamejikita kwenye kufanya ngono na kukaa pamoja bila kupata kile alichotarajia katika uhusiano huo. Mabaki ya mwili wa Celeste yalipatikana Septemba 8, 2025, yakiwa yamewekwa kwenye mifuko miwili ndani ya sehemu ya mbele ya gari aina ya Tesla lililokuwa limekamatwa na polisi karibu na makazi ya Burke.
Daktari wa uchunguzi wa maiti, Grant Ho, aliieleza mahakama kuwa mwili wa Celeste ulikuwa umeharibika sana kiasi cha kushindwa kubaini silaha iliyotumika. Hata hivyo, alisema alikuta majeraha mawili ya kuchomwa yaliyoharibu ini na mbavu, na kuthibitisha kuwa kifo chake kilitokana na mauaji. Burke anakabiliwa na mashtaka kadhaa, yakiwemo ya mauaji na kuharibu mwili wa marehemu.
Kesi hiyo bado inaendelea kusikilizwa mahakamani, na mshtakiwa hajapatikana na hatia hadi mahakama itakapotoa uamuzi wa mwisho.

