Skip to content
PPP TV
THE FEED ⚡

Polisi Arusha Wafungua Milango Ya Ajira Kwa Vijana Wa Mazingira Magumu

LOBy Lucy OgundePPP TV Newsroom · Nairobi · 23 Jul 2026, 12:34 EATPolisi Arusha Wafungua Milango Ya Ajira Kwa Vijana Wa Mazingira Magumu

Ndoto za vijana wanaoishi katika mazingira magumu mkoani Arusha zimeanza kupata mwanga baada ya Jeshi la Polisi kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani humo kuzindua mpango wa kuwabaini na kuwapa mafunzo ya udereva bila malipo, hatua inayolenga kuwajengea ujuzi na kuwainua kiuchumi. Akizungumza leo mara baada ya kufungua mafunzo hayo, Mkuu wa Kikosi cha Usalama barabarani mkoani humo, ACP Zauda Mohamed amesema mpango huo ni sehemu ya mkakati wa kuwawezesha vijana, ili kuwaondoa kwenye mazingira magumu yanayoweza kuwashawishi kujihusisha na uhalifu kwa kuwapatia ujuzi utakaowajengea uwezo wa kujitegemea. ACP Zauda amebainisha kuwa, vijana hao waliwachukua kutoka sehemu mbalimbali ikiwemo vituo vya kulelea watoto wenye changamoto za malezi, maeneo ya kuegesha na kuosha magari, wanaobeba mizigo sokoni pamoja na wapiga debe katika vituo vya mabasi.

Aidha, amefafanua kuwa pamoja na kugharamia mafunzo hayo, Jeshi hilo pia litahakikisha linawasimamia vijana hao katika hatua zote za kupata leseni za udereva ili kuongeza fursa zao za kujiajiri au kuajiriwa mara baada ya kuhitimu mafunzo. Mkuu huyo wa usalama barabarani amemaliza kwa kusema kuwa, anaamini kuwa baada ya vijana hao kuhitimu na kupata leseni zao za udereva, itakuwa ni chachu ya mabadiliko kwao kiuchumi, kuwaondoa katika makundi hatarishi lakini pia kuwaepusha na uhalifu. Naye Godfrey Laizer ambaye ni mnufaika anayejishughulisha na kubeba mizigo amesema mafunzo hayo yamempa matumaini mapya, akieleza kuwa yatamwezesha kupata leseni ya udereva na kufungua fursa za ajira pamoja na kuboresha maisha yake.

Kijana kutoka kituo cha kulelea watoto yatima cha Kindness Children Care Bw. Steven Daniel amelishukuru Jeshi la Polisi kwa fursa hiyo, akisema watajituma katika mafunzo ili kutimiza ndoto zao za badaye. Kwa upande wake Bi.

Emmy Frank anayejishughulisha na kuosha magari amesema mafunzo hayo yatamjengea ujuzi na kumpa nafasi ya kupata ajira zenye kipato bora. Ameahidi kuitumia vyema fursa hiyo na kuzingatia mafunzo yote atakayopatiwa.

WHATSAPPPOST ON XFACEBOOK
YOUR BRAND HERE
Reach 2.5M+ Kenyans daily — advertise on PPP TV · info@triplep.tv
PPP TV NEWSROOM

Reported and written by the PPP TV Newsroom, Nairobi. © PPP TV — Powerful, Precise & Pristine.

MORE STORIES →
© 2026 PPP TV · Powerful, Precise & Pristine · StarTimes Ch. 430