Wabunifu, wasanii na wadau wa sekta ya ubunifu wamehimizwa kujitokeza kushiriki katika Jukwaa la Mashariki Creative Economy Expo 2026, ambalo linalenga kufungua fursa mpya za biashara, ushirikiano na upatikanaji wa masoko kwa kazi za ubunifu ambayo itafanyika kuanzia Agosti 18 hadi 21, 2026 Dar es Salaam. Jukwaa hilo limeandaliwa na Taasisi ya Utamaduni na Maendeleo Afrika Mashariki (CDEA) Akizungumza leo jijini Dar es Salaam Meneja Mradi Kutoka Taasisi hiyo Angela Kilusungu amesema Jukwaa hilo linawakutanisha wabunifu kutoka sekta za filamu, muziki, sanaa za kuona (visual arts), ubunifu wa mambo ya ndani (interior design), uandishi na uchapishaji ili waweze kuonesha kazi zao, kujenga mitandao ya kibiashara na kubadilishana uzoefu unaoweza kuongeza thamani ya kazi zao. Amesema kupitia vikao vya biashara (business conversations), mafunzo na mijadala ya wataalamu, washiriki watapata nafasi ya kujifunza namna ya kuanzisha ushirikiano wenye tija, ikiwemo watayarishaji wa filamu kukutana na watayarishaji wa muziki kwa ajili ya kutengeneza kazi kwa pamoja, jambo litakaloongeza fursa za mapato na kukuza uchumi wa ubunifu.
Kilusungu amebainisha kuwa kwa mara ya kwanza kutakuwepo na dawati maalumu la msaada wa kisheria litakalotoa ushauri kuhusu mikataba, usajili wa hakimiliki, ulinzi wa kazi za ubunifu na namna ya kupanua usajili wa kazi hizo katika masoko ya Afrika. Alisema hatua hiyo itawawezesha wabunifu kulinda kazi zao na kunufaika ipasavyo na mapato yanayotokana na matumizi ya kazi hizo. Amewahimiza wabunifu, wasanii na wananchi kujisajili na kushiriki kwa wingi katika Mashariki Creative Economy Expo 2026, akieleza kuwa jukwaa hilo limeandaliwa mahsusi kuwajengea uwezo, kuwafungulia masoko mapya na kuwaunganisha na wawekezaji pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya ubunifu nchini na Afrika Mashariki.

